http://www.globalpublishers.info/profiles/blogs/dalili-hizi-zinaonesha-una-tatizo-la-kiafya
KWA kawaida mwili ukiwa umepungukiwa aina yoyote ya kirutubisho
(ingredients), huonesha dalili kabla ya kujitokeza kwa ugonjwa. Bahati
mbaya sana, watu wengi hawana uelewa wa dalili hizo. Katika makala haya,
nakutajia dalili chache miongoni mwa dalili hizo.
MIDOMO KUKAUKA
Midomo huakisi afya ya mwili na hali ya maji katika
mwili mzima. Kama una maji ya kutosha mwilini, basi hata midomo yako
itakuwa laini na yenye unyevu. Unapokuwa na upungufu wa maji, ngozi huwa
kavu. Kwa wale akina dada ambao hulazimika kulainisha midomo yao kila
wakati kwa kutumia ‘lip sticks’, wajue kwamba wana upungufu wa maji
mwilini.
Dalili nyingine…
Kuumwa kichwa, kukosa haja ndogo kwa muda mrefu,
kukojoa mkojo wa njano-nyeusi au mkojo wenye harufu kali, ngozi kavu na
unapoiminya ngozi ya nyuma ya kiganja inachelewa kunyooka, nazo ni
dalili kwamba mwili una upungufu wa maji.
SULUHISHO
Kunywa maji ya kutosha kulingana na uzito wa kazi
unazozifanya. Kiwango cha chini ni angalau lita moja ya maji safi na
salama, hakikisha umekunywa maji hata kama husikii kiu. Vile vile ulaji
wa matunda na unywaji wa juisi zitokanazo na matunda au mboga mboga,
huweza kuondoa upungufu wa maji mwilini.
KUKOSA HAJA KUBWA
Kitendo cha kukaa zaidi ya siku moja bila kupata
haja kubwa ni dalili ya wazi ya ukosefu wa kamba lishe (fibre) mwilini.
Kwa kawaida binadamu anatakiwa kupata choo kikubwa kila siku kilicho
laini na kingi. Iwapo hupati choo kila siku na ukipata unapata kigumu,
tena kidogo, jua una matatizo!
Haja kubwa ni muhimu kwa sababu ndiyo
inayosafisha tumbo, uchafu unapokaa tumboni kwa muda mrefu, sumu
zilizomo kwenye haja kubwa hurejea mwilini na husababisha matatizo mengi
ya kiafya, kuanzia magonjwa ya uvimbe, moyo na hata ubongo. Sumu
huvuruga pia mtiririko wa homoni mwilini na hudhoofisha kinga ya mwili.
SULUHISHO
Kula kwa wingi matunda mbalimbali, mboga za majani na
vyakula vitokanavyo na nafaka zisizokobolewa, kama vile ugali wa dona,
mtama, ulezi, n.k. Ulaji wa vyakula hivyo bora, siyo tu kutaondoa tatizo
la ukosefu wa haja kubwa, bali vitakulinda pia dhidi ya magonjwa ya
kisukari, presha, ugonjwa wa moyo na mengine mengi.
VIDONDA PEMBENI MWA MDOMO
Utafiti umeonesha kwamba kupasuka kwa
midomo na kutokea kwa vidonda pembeni ya midomo, huwa ni dalili moja
wapo ya upungufu wa vitamini B mwilini na mara nyingi huwatokea watu
wanaopenda kunywa kilevi kupita kiasi, kula vyakula vya kwenye makopo
(processed foods) na kula sukari kwa wingi.
SULUHISHO
Suluhisho ni kula vyakula vyenye kuongeza vitamin B kwa
wingi. Miongoni mwa vyakula vyenye kiwango kingi cha vitamin B ni pamoja
na kiini cha mayai ya kienyeji, viazi vitamu, nyama ya ng’ombe na ya
kuku, maini na vyakula vitokanavyo na nafaka isiyokobolewa.
Ingawa
unaweza pia kula vidonge lishe vya vitamin B ili kuondoa upungufu huo,
lakini tahadhari lazima ichukuliwe na ina shauriwa kula vyakula vya
kuongeza vitamini hiyo zaidi kuliko vidonge.
No comments:
Post a Comment
HTML tags