WA njia moja au nyingine, unajikuta tumbo limechafuka kwa kujaa gesi,
kuuma na hata kuunguruma, unahisi unahitaji kunywa dawa ili litulie.
Katika makala ya leo utajifunza njia bora ya kutuliza mchafuko wa tumbo
kwa kutumia vyakula badala ya dawa za kisasa ambazo hutuliza dalili na
haziondoi tatizo.
CHANZO
Kabla ya kukimbilia
kwenye tiba, ni vizuri kwanza kujua chanzo cha tatizo na katika hili
unahitaji kujua ni vyakula gani ukila vinasababisha matatizo ya tumbo.
Aina ya vyakula inaweza kutofautiana kati ya mtu na mtu lakini kuna aina
ya vyakula vinajulikana zaidi kusababisha matatizo ya tumbo.
Kwa
mujibu wa Mkurugezni wa Tiba wa Chuo Kikuu cha Tolune. DK. Timothy S.
Harlan (M.D) ambaye pia anajulikana kwa jina la utani kama Dk. Gourment,
vyakula na vinywaji vinavyochangia tumbo kujaa na ukosefu wa choo kwa
muda mrefu huwa ni soda, ulevi (hasa bia), vyakula vyenye mafuta mengi
na vyenye chumvi nyingi.
Kwa mujibu wa Dk. Harlan, vyakula hivyo
vinapoingia tumboni, huwa na tabia ya kuchelewesha usagaji wa chakula na
uondoaji wa uchafu kwenye utumbo, hivyo huwa kikwazo katika mfumo mzima
wa usagaji chakula kwa urahisi.
Ili kujiepusha na matizo ya tumbo ya
muda mrefu na hata kuzuia uwezekano wa kuumwa na tumbo mara kwa mara,
unashauriwa kula vifuatavyo, karibu kila siku ili kulifanya tumbo lako
kuwa safi wakati wote:
PAPAI (PAPAYA)
Baadhi ya
utafiti uliyopo, unaonesha kwamba ‘enzyme’ waliyomo kwenye papai
husaidia usagaji wa chakula tumboni na hivyo kulifanya tunda hili kuitwa
na mtafiti wa zama za kale Christopher Columbus kama ‘tunda la
malaika’.
Watafiti wamebaini kuwa tunda hili, lenye ladha tamu na
harufu nzuri, huboresha mfumo wa usagaji chakula, husafisha utumbo,
huzuia magonjwa ya uvimbe tumboni na huimarisha mfumo wa kinga ya mwili.
“Vitamini
na virutubisho vya papai vina faida nyingi, lakini faida kubwa ya papai
ipo kwenye kirutubisho (Enzyme) aina ya ‘Papain’ ambacho hujulikana kwa
uwezo mkubwa ilionao wa usagaji mzuri wa chakula tumboni,” anasema Dk.
Cari Case mwandishi wa blog ya masuala ya afya.
Mwandishi huyo
anaongeza kwa kusema kuwa papai limekuwa likitumika kama tiba tangu
karne ya 18, lakini utafiti wa kisayansi haukugundua faida za papai hadi
mwaka 1870 wanasayansi walipogundua kirutubisho cha ‘papain kilichomo
kwenye papai na tangu wakati huo tafiti nyingi zimekuwa zikifanywa
kuhusu faida za tunda hili na uwezo wa tiba iliyonalo.
MTINDI (YOGURT)
Hata
kama wewe si mpenzi wa mtindi, jaribu kunywa na utaupenda, hasa uwezo
wake wa kuondoa matatizo ya kujaa gesi tumboni pamoja na matatizo
mengine. Mtindi mzuri ni ule ‘plain’ ambao haujachanganywa na ladha au
vitu vingine kwa lengo la kuongeza ladha. Bakteria asilia waliyomo
kwenye maziwa mtindi ndiyo hufanya usagaji wa chakula kuwa mwepesi.
Mwisho,
ili kupata faida ya papai na mtindi kama ilivyoelezwa hapo juu, ni
vizuri ukala mara kwa mara kama siyo kila siku, kabla au mara baada ya
kula vyakula ambavyo vinaweza kukuletea shida tumboni, au ukaweka mazoea
ya kula kila siku ili kuliweka tumbo lako katika hali salama.
No comments:
Post a Comment
HTML tags