Wednesday, October 5, 2011

TFDA yaonya dawa za kuongeza makalio


MAMLAKA ya Udhibiti wa Chakula na Dawa (TFDA), imewatahadharisha wanawake wanaotumia dawa za kuongeza makalio na ‘hips’ kuwa wana hatari kubwa ya kupata saratani.

Dawa hizo zijulikanazo kama Hip Massage cream ya kuongeza hips, Hip Lift up na Touchmel Hip up cream za kuongeza makalio zilikamatwa na mamlaka hiyo zikiwa zimeingizwa nchini.

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Hiiti Sillo alipokuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru, ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamiieneo la Viwanja vya Mnazi Mmoja.

“Hizi ni kemikali za sumu na lazima wanawake waelewe kwamba kupendwa au kutopendwa na mtu hakutegemei kupaka kemikali,” alisema Sillo.
Alisema dawa hizo zinasababisha kukua kwa nyama hivyo uwezekano wa mtumiaji kupata saratani ni mkubwa.

 Hata hivyo alisema hadi sasa hawajapata taarifa zozote kuhusiana na watu waliopata madhara yaliyotokana na utumiaji wa dawa hizo.
 Mkurugenzi huyo alisema pia wamevitambua vipodozi vingi vyenye viambata vyenye sumu na kwamba wanaendelea kuviondoa sokoni na vingine bado wanaendelea kuvifanyia tathmini.

Alisema ofisi yake inaendelea kufanya uchunguzi wa dawa zingine zilizotiliwa shaka kwani zipo ambazo hawazitambui na hawajazisajili, lakini walizikamata kwenye soko.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo alisema wanatarajia nchi mbalimbali zitakuja kufanya uchunguzi wa sampuli za bidhaa mbalimbali baada ya kuwa na maabara inayokidhi vigezo vya kimataifa.Kwa mujibu wa Sillo, maabara hiyo ni ya sita katika Bara la Afrika na kwamba ni kati ya maabara 19 zinazotambuliwa duniani na kukidhi vigezo vya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mkurugenzi huyo alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa dawa bandia kwani wanaofanya biashara hiyo na vyakula ambavyo si salama wako miongoni mwa wananchi.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

HTML tags

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...